Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Friday, 20 February 2015

DKT.SHEIN AONGOZA MAZISHI YA SALIMIN AWADH SALIMIN.


Mwili wa Marehemu Salmin Awadh  ukiingizwa  katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani kwa ajili ya kuagwa rasmi.
Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji akiongoza  waumini katika Sala ya Marehemu Salmin Awadh Salmin katika Masjid Noor Muhammad (SAW) uliopo Mtaa wa Kwamchina mwanzo. (Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar)
 Rais mstaafu wa Zanzibar, Dkt.Amaan Abeid Karume akisalimiana na makamo wa rais wa Tanzania Dkt.Mohamed Ghalib Bilal.
Naibu Katibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai  na Mwakilishi wa Jimbo la Kikwajuni Mahmoud Muhammed wakibadilisha mawazo kuhusu msiba huo. (Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar). 
Mamia ya wananchi waliohudhuria sala ya kumuombea Marehemu Salmin Awadh Salmin wakiutoa msikitini mwili wa marehemu kuelekea kijijini kwao Makunduchi kwa mazishi.


Na George  Simba, Zanzibar.

    RAIS wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein ameungana na Mamia ya wananchi katika mazishi ya aliyekuwa mwakilishi wa jimbo la magomeni Zanzibar, Salimin Awadh Salimin huko katika kijiji cha kijini Makunduchi Mkoa wa kusini Unguja...


Marehemu Awadhi ambaye pia alikuwa mnadhimu wa wajumbe wa baraza hilo kutoka CCM na mjumbe wa kamati ya uongozi wa baraza hilo, alifariki  juzi mchana baada ya kuugua hafla mara baada ya kumalizika kwa kikao cha sekretarieti ya chama hicho kilichofanyika katika ofisi kuu ya CCM, Kisiwandui Zanzibar.

Mapema mwili wa marehemu kabla ya kupelekwa kijijini kwao kwa ajili ya mazishi ulipelekwa katika baraza la wawakilishi Zanzibar ililopo Mbweni Mjini hapa kwa ajili ya kuagwa na kupewa heshima ya mwisho na wawakilishi pamoja na watendaji wa baraza hilo wakiongozwa na Naibu spika wa baraza la wawakilishi Ali Abdalla Ali.

Baadae mwili huo uliingizwa katika ukumbi wa baraza hilo ambao mbali na wajumbe wa baraza hilo pia lilikuwa na viongozi kadhaa akiwemo makamo wa rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dkt, Mohamaed Ghalib Bilal ,  makamo wa kwanza wa rais wa Zanzibar maalim seif sharif hamad, makamo wa pili wa rais balozi seif ali idi, jaji mkuu wa Zanzibar omar Othman makungu, waziri mkuu mstaafu wa Tanzania Edward Lowasa na waziri.

Viongozi wengine ni pamoja na Adam Malima, mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho Setiven Wasira na  viongozi wengine wa chama na serikali  ambapo kabla ya dua ya kumuombea marehemu msaididi wa katibu wa mufti wa Zanzibar sheikh thabit nouman jongo aliwaasa wananchi hao kukumbuka kifo wakati wote ili kujiweka katika mazingira mazuri hapa duniani na kesho akhera.

Akitoa salamu za chama cha mapinduzi kwa niaba ya Katibu mkuu wa CCM Taifa Omar Kinana ambaye kwa sasa yupo nchini Sudan Juba, Naibu katibu mkuu wa chama hicho Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema kuwa toka kutokea kwa msiba huo chama hicho kimepata pengo kubwa linalotakiwa kuzibwa na viongozi wengine watakaoenzi fikra za Salimin kwa vitendo.

Alisema kuwa marehemu alipata mauti akiwa katika utekelezaji wa kazi za kichama hivyo katika uhalisia amekufa kishujaa ndani ya uwanja wa kisiasa pia tunatakiwa kumukumbuka kwa wema na mchango wake.

“Nakumbuka siku ya mauti yake katika kikao cha sekretelieti marehemu alitoa hoja na michango mizuri huku akiimiza umoja na mshikamano na kuimarisha muungano wetu.”alisema Vuai.

Kwa upande wa baraza la wawakilishi akisoma wasifu wa marehemu, Msaidizi wa katibu mkuu wa baraza hilo Amour Haji Nassor alisema marehemu Salimin Awadh Salimin alizaliwa  Juni 6, 1958 katika kijiji cha Kijini mkoa wa kusini Unguja na kupata elimu yake ya msingi katika skuli ya makunduchi kati ya mwaka 1963 na 1967 labla ya kujiunga na skuli ya makunduchi kwa ajili ya masomo ya sekondari kati ya mwaka 1968 na 1970.
                      
Aidha alieleza marehemu alianza harakati za kisiasa mwaka 1995-2000 akiwa kama diwani na kuingia baraza la wawakilishi mwaka 2005 na kupata nafasi mbali mbali zikiwemo  mwenyekiti wa kamati  ya kudumu ya fedha mnamo mwaka 1971 hadi 1974 hadi 1982 alipata mafunzo ya uongozi katika jeshi la wananchi katika ngazi mbali alijiunga na chuo cha uchumi Zanzibar na kupata cheti cha fani hiyo.

Pia mwaka 2010 hadi mwaka 2015 alikuwa ni mnadhimu wa wawakilishi wa CCM katika baraza la wawakilishi Zanzibar.

Marehemu ameacha kizuka mmoja na watoto saba ambapo familia yake kwa sasa inaishi visiwani Zanzibar.

 Aidha mbali ya kuwa mnadhimu na mnamo mwaka 2010 aliteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya shirika la magazeti y serikali dhamana ambayo alikuwa nayo hadi anafariki na ameacha mke ana watoto saba.

 Akimzungumzia marehemu huyo waziri kiongozi mstaafu wa Zanzibar Shamsi Vuai Nahodha alisema marehemu Awadhi alikuwa ni kiongozi shupavu aliyekuwa imara katika kujenga hoja na kuisimamia kwa lile jambo aliloliamini jambo ambalo alikuwa anaweza kufanikisha mambo yake bila ya vikwazo.

Alisema katika muda wote toka awe karibu na marehemu alikuwa  ni mmoja wa watu wenye mchango mkubwa katika kukuza utawala bora ndani ya baraza la wawakilishi kwa michango yake na kuisimamia serikali bila ya kujali dhamana yake ndani ya chama.

“Katika maisha ya kisiasa nimeweza kujifunza mambo mengi kutoka kwa marehemu salimin kwani alikuwa ni mtu mwenye kujenga hoja za maendeleo na kuzisimamia bila ya woga. ”, alisema Nahodha.

Aidha alisema kuwa miongoni mwa sifa ya marehemu alikuwa ni mkweli wala hakuwa na sifa ya kupindisha ukweli ndio maana alikuwa anaaminiwa na chama cha mapinduzi kwa wakati wote.

Kwa upande wake  Mjumbe wa kamati kuu ya CCM Taifa, Steven Wasira alisema kuwa chama cha mapinduzi kwa ujumla kimepata pigo na pengo kwa kuondokewa na marehemu Salimin kwani alikuwa ni mfano wa kuigwa kutokana na weledi pamoja na mikakati yake katika utendaji mbali mbali wa majukumu yake.

“Nimeanza kumuelewa zaidi alipokuwa katika kamati kuu na kugundua kuwa Awadhi alikuwa ni kiongozi hodari na mwenye weledi  mkubwa  pia hata wakati wa bunge maalum la katiba marehemu ni miongoni mwa viongozi wa CCM waliovusha jahazi la kupatikana kwa katiba inayopendekezwa. ”, alisema Waziri huyo.

Naye Mlezi wa chama cha ADC, ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Wawi Pemba, Hamad Rashid Mohamed alisema kuwa kifo cha  Kiongozi huyo kimepokelewa kwa majonzi makubwa ndani ya chama hicho kwani alikuwa ni mwanasiasa aliyekuwa ni mtetezi na msimamizi mzuri wa maslahi ya Zanzibar.

“Marehemu anastahiki kukumbukwa kama shujaa wa Zanzibar kwani ameweza kuleta historia ya kipekee katika uwanja wa kisiasa hapa visiwani pia ni alikuwa ni mtu mwenye ushirikiano.”alifafanua Hamad.

Nae Mwakilishi wa jimbo la Ole Pemba wa Tiketi ya CUF, Hamad Masoud alisema kuwa umakini wa marehemu salmini ni kitu pekee kitakachokosekana ndani ya baraza hilo wakati huu kuwataka wajumbe wote kuungana na kuyasimamia mtakwa ya marehemu ya kuwa ba bararaza linalowawakilisha wananchi badala ya vyama vyao.
                
“Bado wanasiasa tunayo nafasi ya kujitahimini kwa yale tunayofanyia wananchi wetu kwani Marehemu alikuwa ni miongoni mwa wanasiasa waliokuwa wawazi na wakweli katika kusimamia sera na milengo ya chama chake sambamba na kutekeleza mipango ya serikali kupitia baraza la wawakilishi.”, alisema masoud.


Mwili wa marehemu kabla ya kupelekwa kijijini kwao Kijini kwa maziko, majira ya saa sita mchana ulipelekwa katika msikiti wa Noor Muhhammad uliopo Mombasa kwa Mchina kwa ajili ya kuswaliwa, sala ambayo ilitanguliwa na sala ya Ijumaa na kuhudhuriwa umati mkubwa wa wananchi na viongozi mbali mbali walioongozwa na Makamo wa Rais dkt. Mohammed Gharib Bilal na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Shein.

Katika maisha ya kisiasa marehemu Salimin aliwahi kujenga hoja mnamo  Mei 4, mwaka jana, Salmin alisema wawakilishi wa CCM wanajiandaa kuwasilisha hoja binafsi kwenye Baraza la Wawakilishi ili kuwapa nafasi wananchi waulizwe iwapo wanataka kuendelea na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), au la.


Kauli hiyo aliitoa wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa chama hicho ulioongozwa na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana kwenye viwanja vya Kibandamaiti, Unguja. 


Salmin alisema wajumbe hao wamefikia hatua hiyo kwa kuwa wanaona kwamba lengo na matumaini ya kuundwa SUK yamefutika na hayana dalili njema katika siku za usoni.


Alisema ni vyema wananchi wakaulizwa kama bado wana hamu na mfumo huo au ule wa zamani urejeshwe.


Katika mkutano huo, alimwomba Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kuunga mkono hoja hiyo itakapowasilishwa ili kutoa nafasi mpya ya kidemokrasia kwa wananchi wake kujua kama wanataka mfumo wa sasa au wa zamani.


Lakini kwa upande wa vyama vya upinzani hasa CUF hoja hiyo waliipinga na kumwona kiongozi huyo kama msaliti wa amani visiwani Zanzibar lakini msimamo huo alikuwa akiusisitiza kwa kujenga hoja kuwa SUK  lazima ipigiwe kura tena na wananchi.

No comments:

Post a Comment

 
 
Blogger Templates