Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Tuesday, 17 March 2015

SMZ: YASEMA KVZ HAIJAVAMIA ENEO LA WAWEKEZAJI.

Na Miza Kona na Maryam Kidiko-Maelezo Zanzibar.

  SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ) hakijavamia eneo la Mwekezaji wa Kiwanda cha Sukari Mahonda...

Hayo yamesemwa leo huko Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Wilaya ya Magharibi Unguja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum mhe. Haji Omar Kheri wakati akijibu suala la Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni Mhe. Jaku Hashim Ayoub aliyetaka kujua kwa sabaabu gani Kikosi cha Valantia Zanzibar kimevamia eneo la uwekezaji.

Amesema maeneo hayo tayari yameshapimwa na serikali kwa ajili ya matumizi ya Kikosi hicho na eneo hilo  sio la kiwanda cha sukari pia kiwanda hakina haki ya kisheria ya kulitumia.

 “Eneo hilo limepimwa na kwa sasa si sehemu ya shamba la miwa la kiwanda cha Sukari Mahonda na Uongozi wa kiwanda cha Mahonda unaelewa kuwa sio sehemu yao”, amefahamisha Waziri huyo.

Amesema kuwa eneo hilo limekuwa la kiulinzi ambalo lilikabidhiwa kikosi cha Valantia (KVZ) kwa ajili ya kuanzisha Kambi ya Pangatupu ili kuimarisha shughuli za ulinzi katika maeneo hayo.

Ameeleza kuwa Serikali imeandaa mpango maalum wa kuwapatia eneo jengine kwa ajili ya kuweza kujiendeleza na shughuli zao za kiwanda hicho ili kuepukana na upungufu na usumbufu wa maeneo ya mashamba ya miwa na kudhorotesha uzalishaji kwa wawekezaji hao.

Wakati huo huo Naibu Waziri wa Miundo Mbinu na Mawasiliano Mhe. Issa Haji Gavu amesema Serikali kupitia Program ya ZUSP inayotekelezwa kupitia Wizara ya Fedha inakusudia kujenga mitaro ya maji katika maeneo mbalimbali ya mji wa Zanzibar ikiwemo eneo la Kijangwani ili kuondoa kutuama kwa maji wakati wa mvua katika eneo hilo.

Akijibu suala laMwakilishi wa Jimbo la Kwahani Mhe. Ali Salum Haji aliyetaka kujua Wizara imejipanga vipi kumaliza tatizo hilo, Naibu huyo amesema kuwa eneo hilo la barabara iliyopo mbele ya jengo la Posta, Kijangwani wakati wa mvua hujaa maji ambayo huwa ni kero kwa wananchi ambao hutumia maeneo hayo kwa shughuli zao.


Ameeleza kuwa tatizo la kutuama maji linatokana na eneo hilo kukosa mitaro yenye uwezo wa kuchuku maji yanayokusanyika hapo kutoka maeneo yajuu kwa vile eneo hilo asili yake lipo bondeni.    

No comments:

Post a Comment

 
 
Blogger Templates